ZINGATIENI SHERIA, KATIBA NA KANUNI YA VYAMA VYENU - MUTUNGI.

Na: Mwandishi Wetu, ORPP.
Viongozi wa Vyama vya Siasa nchini watakiwa kuzingatia Sheria na Katiba za nchi sambamba na kuzingatia kanuni na miongozo iliyopo katika Katiba za vyama vyao ili kuepuka migogoro miongoni mwao.
Wito huo umetolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa(RPP), Jaji Francis Mutungi alipokuwa akitoa salama zake mbele ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza hilo kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Nashera Hoteli Manispaa ya Morogoro leo tarehe 14 Mei 2025.
Akizungumza katika kikao hicho Jaji Mutungi amewataka wajumbe wa Baraza la vyama vya siasa nchini kuhakikisha wanazingatia Sheria za nchi, Kanuni na Katiba za vyama vyao ili kuepuka migogoro na migongano ya kisiasa ambayo husababisha kuwepo kwa hali mbaya ya kisiasa nchini.
Aliongeza kuwa wanachama wa vyama vya siasa wanawajibu wa kuzingatia sheria za nchi kanuni na katiba za vyama vyao ili kuhakikisha wanafanya yaliyo sahihi ili kuondokana na migogoro ndani ya vyama na kuhakikisha maendeleo yanafanyika ndani ya chama na nje ya chama.
".Nawasihi mzingatie Sheria za nchi, mzingatie katiba za vyama vyenu na sheria zinazosimamiwa na Baraza la vyama vya siasa.." ameisisitiza Jaji Mutungi.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia Baraza la Vyama vya siasa imeandaa kikao cha siku mbili cha kawaida cha baraza hilo kuanzia tarehe 14 – 15 Mei, 2025, ambapo pamoja na agenda za kawaida wajumbe wanapata fursa ya kujengewa uelewa katika masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyotolewa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) na namna ya kuanzisha sera za jinsia na uendeshaji wa dawati la jinsia katika vyama vyao itakayotolewa na taasisi ya WiLDAF.