Umoja wa Kitaifa ni Muhimu Katika Utekelezaji wa Dira 2050 - Waziri Deus Sangu
Na: Mwandishi Wetu
Serikali imeviasa vyama vya siasa kuendela kuimarisha mazungumzo, ushirikiano na umoja wa kitaifa wakati Tanzania ikijiandaa kuanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwezi Julai mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, wakati akifungua warsha ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa mjini Morogoro tarehe 17 Juni 2026. Warsha hiyo yenye lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu jukumu jipya la Mahusiano ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa siasa.
Kwenye hotuba yake Waziri Sangu amesema vyama vya siasa ni wadau muhimu katika kukuza amani, umoja na ustawi wa jamii. Ameongeza kuwa, utayari wao wa kushirikiana na Serikali ni muhimu katika kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo vyama vya siasa vyenyewe.
Amewapongeza na kuwaasa viongozi wa kisiasa kuendelea kuwa mabalozi wa amani na kutokubali kutumiwa na watu wachache wenye maslahi binafsi wanaoweza kuligawa taifa au kuhatarisha utulivu na amani ya nchi.
“Leo tunapozungumzia mahusiano kati ya Serikali na vyama vya siasa, niwahakikishie kuwa dhana hii inaendelea kutekelezwa kupitia falsafa maarufu ya 4R iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kujenga taifa lenye amani na umoja,” alisisitiza Waziri Sangu.
Amesema falsafa hiyo ya Rais Samia ya 4R, ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Ujenzi Upya, inaendelea kuongoza jitihada za Serikali katika kukuza mazungumzo, kuimarisha kuaminiana na kujenga taifa lenye umoja kupitia ushirikishwaji mpana.
Waziri Sangu amelipongeza Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuendelea kushirikiana na Serikali, ikiwemo kutoa ushauri katika masuala mbalimbali ya kitaifa. Amesema ushirikiano huo ni muhimu wakati nchi ikielekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inahitaji mshikamano na malengo ya pamoja bila kujali tofauti za kisiasa.
Akiunga mkono ujumbe huo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Mhe. Juma Ali Khatibu, amesema vyama vya siasa vina nafasi kubwa katika jamii ya Watanzania na vinaweza kusaidia kuimarisha mahusiano, amani na maelewano ndani ya jamii.
Khatibu ameongeza kuwa Baraza hilo linatambua dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza siasa za ushirikishwaji. Ametolea mfano uteuzi wa mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo, Dkt. Eveline Wilbard Munisi kutoka NCCR-Mageuzi, kuwa Mbunge na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano. Amesema uteuzi huo unaonesha kuaminiana, ushirikishwaji na ushirikiano katika siasa za ushindani nchini.
Akieleza zaidi kuhusu lengo la kikao hicho, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mstaafu Francis Mutungi, amesema warsha hiyo ni matokeo ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vyama vya Siasa kilichofanyika tarehe 21 Mei mwaka huu. Amesema katika kikao hicho ilikubalika kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itoe mada ya kujenga uelewa kuhusu jukumu jipya la Mahusiano kwa ustawi wa Tanzania.
Warsha hiyo imehudhuriwa na viongozi wa kitaifa kutoka vyama vya siasa 18 kati ya 19 vyenye usajili kamili. Kikao hicho kinaonesha dhamira ya Serikali ya kuviona vyama vya siasa si tu kama washindani wa uchaguzi, bali pia kama washirika muhimu katika ujenzi wa amani, mshikamano wa jamii na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.