Ruzuku ya Serikali
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ndio yenye jukumu la kugawa ruzuku ya kila mwezi kwa vyama vya siasa vyenye sifa kwa mujibu wa Sheria.
Ruzuku ya vyama vya siasa ni fedha zinazotolewa na Serikali kwa vyama vya siasa kwa ajili ya kusaidia shughuli za uendeshaji wa vyama hivyo. Vyama vinavyopata ruzuku ni vile vilivyopata angalau asilimia tano ya kura zote halali zilizopigwa katika Uchaguzi Mkuu na vyama vyenye Wabunge au Madiwani.
Kigezo kinachotumika ili chama kiweze kupata ruzuku ni kuangalia matokeo ya uchaguzi kuona kama chama kimepata asilimia tano ya kura au kama chama kimeshinda nafasi za ubunge au udiwani, kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 16 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, namba 5 ya mwaka 1992.
Chama kinachopata ruzuku kinaweza kupoteza sifa ya kupata Ruzuku iwapo kitapoteza kwa namna yoyote ile mbunge au diwani anayepelekea chama hicho kupata ruzuku. Pia chama kitapoteza sifa iwapo kitafutiwa usajili wake wa kudumu. Chama kikipoteza sifa ya kupata ruzuku kitaondolewa kwenye orodha ya kupata ruzuku.