Viongozi wa Siasa Tayari Kuwa Vinara wa Majadiliano
Viongozi wa vyama vya siasa wameeleza utayari wao wa kuunga mkono majadiliano ya pamoja kati ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni hatua inayotarajiwa kuimarisha amani, ushirikiano, utulivu wa kijamii na mshikamano wa kitaifa.
Utayari huo umebainishwa mjini Morogoro wakati wa kikao kilichowakutanisha Ofisi ya Waziri Mkuu inayosimamia Kazi, Ajira na Mahusiano na wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa.
Kikao hicho kilitoa fursa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kutambulisha majukumu ya Idara ya Mahusiano na kueleza nafasi yake katika kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, makundi ya kijamii na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Mauhusiano, Bi. Zuhura Yunus, amesema kikao hicho ni sehemu ya jitihada zinazoendelea za kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na wadau wake kupitia majadiliano, ushirikiano na uelewa wa pamoja.
Amesema vyama vya siasa ni wadau muhimu katika kujenga uaminifu, kuimarisha mawasiliano na kuendeleza umoja wa kitaifa, hasa kutokana na ukaribu wao na wananchi katika ngazi mbalimbali za jamii.
Akiendeleza ujumbe huo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mstaafu Francis Mutungi, amesisitiza kuwa vyama vya siasa ni washirika muhimu katika kulinda amani na utulivu nchini. Amesema mahusiano mazuri kati ya Serikali na wadau wa siasa hujenga ushirikiano, na ushirikiano huo hufungua nafasi ya majadiliano na upatikanaji wa suluhu za changamoto mbalimbali za kijamii na kitaifa.
Jaji Mutungi ameongeza kuwa viongozi wa siasa wana nafasi kubwa ya kulinda tunu ya amani ya Tanzania kwa kuhamasisha umoja, uvumilivu na ushiriki wa wananchi kwa njia ya staha na uwajibikaji.
Kauli ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na vyama vya siasa pia imeungwa mkono na Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma, CHAUMMA, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Baraza la Vyama vya Siasa, Bw. Salum Mwalimu.
Amepongeza kikao hicho akisema ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano, huku akisisitiza kuwa mahusiano mazuri kati ya Serikali na wadau wa siasa ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vya kitaifa, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Zaidi ya kubadilishana mawazo, kikao hicho kinatarajiwa kuboresha mawasiliano kati ya Serikali na wadau, kuimarisha imani kati ya taasisi za umma na viongozi wa siasa, pamoja na kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano katika kushughulikia masuala ya maendeleo ya taifa.
Kikao hicho cha siku moja kiliandaliwa kufuatia ombi la Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukutana na wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa ikiwa na lengo kutoa elimu kuhusu majukumu ya Idara hiyo mpya ya Mahusiano