VYAMA VYA SIASA NA WADAU WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MATAKWA YA SHERIA YA GHARAMA ZA UCHAGUZI
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mhe. Jaji Francis S.K. Mutungi amevikumbusha Vyama vya Siasa na Umma kwa ujumla kuhusu utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Gharama za uchaguzi.
Hayo ameyasema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Julai 17, 2018 ikiwa ni maandalizi ya tukielekea kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Buyungu na kata 77 utakaofanyika tarehe 12 Agosti, 2018.
Jaji Mutungi amesema kuwa Sheria ya Gharama za uchaguzi inamtaka kila Mgombea wa Ubunge na Udiwani kuweka wazi mapato na matumizi ya gharama anazotarajia kuzitumia wakati wa uchaguzi husika kwa kujaza fomu maalumu ( EE1 & EE2) ambazo hujazwa na kuwasilishwa kwenye mamlaka husika ndani ya siku saba, kuanzia siku ya uteuzi wa wagombea. Hivyo anasisitiza ujazaji sahihi wa fomu hizo maalumu ili kukidhi matakwa ya Sheria.
Pia, Jaji Mutungi amewataka wagombea, vyama vya siasana umma kwa ujumlakuepuka kufanya vitendo vinavyokatazwa na Sheria za nchi hususani Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki na pia unaendeshwa katika hali ya Amani na utulivu.
Sheria ya Gharama ya uchaguzi ni Sheria inayosimamia mapato na matumizi ya fedha zote ambazo zinatarajiwa kutumika na ambazo zimetumika kwa ajili ya uteuzi, kampeni za uchaguzi na shughuli za uchaguzi kwa chama cha siasa, mgombea, Asasi na Serikali. Sheria hii ilianzishwa mwaka 2010 ikiwa na lengo la kudhibiti matumizi ya gharama za uchaguzi na vitendo vinavyokatazwawakati wa mchakato wa uteuzi, kampeni na uchaguzi na pia kuweka uwanja sawa wa kisiasa miongoni wa vyama vya siasa.