JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

Msajili wa Vyama vya Siasa Asisitiza Amani wakati wa Kampeni za Wagombea kueleke Uchaguzi Mkuu Oktoba,29
05 Sep, 2025
Msajili wa Vyama vya Siasa Asisitiza Amani wakati wa Kampeni za Wagombea kueleke Uchaguzi Mkuu  Oktoba,29

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Bibi. Edina Assey kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Saisa, amefanya kikao elekezi na Wenyeviti pamoja na Makatibu wa Wilaya wa vyama vya siasa katika Wilaya ya Ulanga. Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kutoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

Katika kikao hicho, Msajili aliwafafanulia washiriki majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, sheria na kanuni zinazowaongoza, pamoja na haki na wajibu wa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kuhakikisha kampeni zinazoendeshwa zinakuwa za amani, zenye kuheshimiana na zinazodumisha misingi ya demokrasia, ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia bila bughudha wala uvunjifu wa amani.

Msajili aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa wakati huu wa kampeni ni muda wao  kuwa mabalozi wa amani na mshikamano wa kitaifa kwa kutanguliza hoja za sera na mawazo yenye kujenga taifa badala ya maneno ya uchochezi, kwani uchaguzi wa amani ndio msingi wa maendeleo na mshikamano wa Watanzania wote.