JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

VYAMA VYA SIASA KUJENGEWA UWEZO UANDAAJI SERA ZA JINSIA NA UTUNZAJI WA REJESTA ZA VIONGOZI WA VYAMA
08 May, 2026
VYAMA VYA SIASA KUJENGEWA UWEZO UANDAAJI SERA ZA JINSIA NA UTUNZAJI WA REJESTA ZA VIONGOZI WA VYAMA

Na: Mwandishi Wetu - ORPP

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Africa (WILDAF), ipo katika mchakato wa kuvijengea uwezo vyama vya siasa kuhusu masuala ya sera za jinsia, uundaji wa madawati ya jinsia ili vikidhi matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2024, sera ya jinsia na sheria zingine za nchi.

Hayo yamebainishwa  na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Ndg. Sisty Nyahoza wakati akizungumzia tathmini ya ziara hiyo iliyofanyika jana tarehe 7 Mei, 2026 katika Ofisi za  Chama cha Sauti ya Umma (SAU) zilizopo Magomeni Kondoa  jijini Dar es Salaam.

 “Tupo katika zoezi la kutembelea vyama vya siasa ili kuvisaidia katika utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa kuhusu masuala ya jinsia na uundwaji wa madawati ya jinsia, vilevile ni kuangalia ni jinsi gani wanatekeleza masharti ya sheria ya vyama vya siasa kuhusu rejista za viongozi wa vyama vya siasa” Alisema Nyahoza.

Nyahoza aliongeza kuwa zoezi hili linasaidia sana vyama vya siasa kuwa na uelewa masuala ya jinsia na kwamba vinahitajika kuwa na sera za jinsia ili kuwe na msukumo wa ndani wa kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa na wanaume katika kushiriki masuala ya kisiasa na uongozi katika vyama vya siasa na serikali. 

Kwa upande wake Ofisa Mradi kutoka  Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Africa (WILDAF), Bi. Mkula Joseph Mandago amesema kuwa kupitia shirika lao wanatekeleza mradi unaoitwa Wanawake Sasa wenye lengo la kuhakikisha mwanamke anaweza kushiriki katika ngazi za maaumuzi michakato ya kidemokrasia pamoja na masuala yote yanayohusiana na uongozi.

Bi. Mkula ameeleza kwamba kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wamekuwa wakitekeleza jukumu ikiwa ni pamoja na kuvijengea uwezo vyama vya siasa katika kuhakikisha vinakuwa na sera za jinsia na uanzishwaji wa madawati ya jinsia ambapo katika ziara hii lengo ni kubaini mahitaji ya vyama vya siasa ili ifikapo tarehe 25 Mei, 2026 vyama vyote viwe na sera hizo pamoja na madawati hayo.

“Tunaendelea na ziara hii lengo likiwa vyama vyote viwe na sera za jinsia pamoja na madawati ya jinsia ifikapo tarehe 25 Mei, 2026 kwani baada yah apo kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tumepanga kuratibu mafunzo kwa wajumbe wote watakao kuwa wanaunda na kuratibu madawati ya jinsia” alisisitiza Mkula.

Zoezi hili la kutembelea Ofisi za vyama vya siasa linafanyika kwa siku 10 kuanzia tarehe 5 hadi 16 Mei, 2026 ambapo mpaka sasa jumla ya vyama sita vimeshatembelewa ambavyo ni UDP, CHAUMMA, MAKINI, ADA TADEA, TLP na SAU.

slot gacor