JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

Mahakama Yampa Ushindi Msajili, Madai ya IPP Yakwama
17 Aug, 2026
Mahakama Yampa Ushindi Msajili, Madai ya IPP Yakwama

 

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imethibitisha uhalali wa hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutokipa usajili wa muda Chama cha Independent People’s Party (IPP), baada ya kubaini kuwa hakikukamilisha masharti muhimu ya kisheria ambayo yangeweza kuhalalisha maombi hayo. 

Uamuzi huo uliotolewa Agosti 14, 2026 na Jaji wa Mahakama Kuu, Arnold Kirekiano, katika Maombi ya Mapitio ya Kimahakama Na. 3005 ya mwaka 2026, yaliyofunguliwa na waasisi wawili wa IPP, Vyonheaven Urima na Andrew Bomani.

Waasisi hao walidai kuwa walikuwa wametimiza masharti yote na kwamba Msajili alikuwa na wajibu wa kukisajili chama hicho. Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa, kupitia Msajili Msaidizi Sisty Nyahoza, aliieleza kuwa maombi hayo yalikuwa na upungufu katika fomu za kisheria, katiba na kanuni za kuendesha chama, uthibitisho wa uraia na wasifu wa mmoja wa waasisi.

Mahakama ilibaini kuwa Ofisi ya Msajili iliwaeleza waombaji upungufu huo na kuwapa nafasi ya kuyarekebisha. Hivyo, hakukuwa na ushahidi kwamba Msajili alikiuka mamlaka yake au alishindwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria.

Jaji Kirekiano alisema wajibu wa Msajili kukisajili chama huanza pale tu waombaji wanapowasilisha maombi halali na kutimiza masharti yote ya sheria.

Alisisitiza kuwa mapitio ya kimahakama si rufaa. Mahakama haiwezi kuamua upya masuala yaliyo ndani ya mamlaka ya Msajili; jukumu lake ni kuchunguza iwapo mamlaka hiyo ilitumiwa kwa kufuata sheria au vinginevyo.

Kwa uamuzi huo, Mahakama imeweka wazi kuwa nia ya kuanzisha chama peke yake haitoshelezi masharti ya kisheria na waombaji wanalazimika kukamilisha mchakato mzima kama ulivyoainishwa kwenye sheria.

slot gacor