Watumishi ORPP Wakumbushwa Matumizi Sahihi ya Vifaa vya TEHAMA
Na: Mwandishi Wetu, ORPP
Watumishi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa watakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA na kuwa makini wanapokuwa katika mitandao ya kijamii ili kuhakikisha wanalinda unyeti wa ofisi hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi wakati akifungua mafunzo ya TEHAMA Juu ya Matumizi Bora , Sahihi na Usalama wa Vifaa, Data na Mifumo ya TEHAMA Serikalini leo jijini Dodoma.
“ Inawezekana kabisa kwamba baadhi ya watumishi wakachukulia kuwa mafunzo haya ni ya kawaida lakini niseme tu kuwa mafunzo haya ni msingi imara na silaha ya usalama wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.” Alisema Jaji Mutungi.
Aidha Jaji Mutungi aliongeza kuwa mafunzo haya ni utekelezaji wa Sera ya TEHAMA na Sera ya Usalama wa TEHAMA ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambapolengo la kuu ni kuhakikisha tunalinda usalama wa taarifa zote dhidi ya mashambulizi kutoka ndani na nje ya Taasisi yanayoweza kujitokeza aidha kwa kukusudia au kwa bahati mbaya.
Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu huo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia Kitengo cha Habari, Mawasiliano, Teknolojia na Takwimu (ICT &Statistic Unit iliona ipo haja ya kuwajengea uwezo watumishi wake ili kujiweka tayari kukabiliana na changamoto za matumizi ya vifaa vya Tehama na mitandao.
Mafunzo haya ya siku mbili ambayo yanashirikisha watumishi wote wa Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa yanafanyika kuanzia leo tarehe 24 na 25 Januari 2024 katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.