Wanasia Waache Propaganda, Wausome Vizuri Mswada
Serikali inawaonya Wanasiasa kuacha propaganda za kupindisha ukweli na kutoa tafsiri potofu kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2018 kwa lengo la kuuhadaa umma kukataa muswada bali watumie fursa hii baada ya kuusoma , kutoa maoni yao stahiki kwa lengo la kuuboresha .
Kauli hiyo imetolewa jana Desemba 20, 2018 na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa Bw. Sisty Nyahozawakati wa mahojiano ya moja kwa moja naBBC Swahili kwenye kipindi chaDira ya Dunia kilichorushwa 20 Desemba 2018 saa tatu usiku.
Akijibu swali lililoulizwa kuhusiana na Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia shughuli za chama cha siasa kwa kumsimamisha mwanachama wa chama cha siasa uanachama, amesema suala hilo halina ukweli wowote bali kifungu kinampa Msajili mamlaka ya kumsimamisha mwanachama wa chama cha siasa kufanya siasa kwa muda utakaowekwa kama atakiuka sheria na si kumsimamisha uanachama.
Nyahoza alisisitiza kuwa malalamiko ya wanasiasa kwa sasa hayana msingi wowote kwa sababu lengo la Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa 2018 ni kuboresha Sheria ya Vyama vya Siasa iliyopo sasa ili kukidhi mahitaji ya wakati huu, kwendana na wakati na pia kuondoa changamoto zilizopo.
“Swala la msingi kwa sasa ni kuwaasa wanasiasa waache kupindisha na kutoa tafsiri potofu kuhusu muswada huo kwa lengo la kuhadaa umma ili wadau/wananchi waukatae muswada bali watumie fursa hii baada ya kuusoma kuwasilisha maoni yao kwenye kamati ya bunge ambayo itakaribisha maoni ya wadau kwa lengo la kuuboresha badala ya kuendekeza propaganda zisizo na tija” aliendelea kusisitiza.
Maoni ya wadau kuhusiana na muswada huu yalianza kukusanywa mwaka 2013 na wadau wakuu ambao ndio vyama vya siasa walishirikishwa kutoa maoni yao. Vyama viliwasilisha maoni yao kwa chama kimoja kimoja na pia kupitia mijadala kwenye vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa .