VYAMA VYA SIASA VYATAKIWA KUZINGATIA MASLAHI MAPANA YA TAIFA
Viongozi wa kitaifa wa vyama vya Siasa nchini wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa maslahi mapana ya taifa kuepuka kuanzisha vyama kwa maslahi binafsi.
Hayo yalisemwa Jana na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe. Mohammed Ally Ahmed wakati wa kufunga mafunzo kwa viongozi wa kitaifa ya vyama vya Siasa yaliyofanyika kwa siku mbili katika ukumbi mdogo wa Ofisi za Bunge Septemba 19 na 20 , 2018 kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao ili kuendesha vyama vyao kama taasisi.
“Linapotokea zuri basi tuseme hili ni zuri na linapotokea baya tuseme hili lina tatizo kwa maslahi mapana ya taifa letu, utitiri wa vyama vya siasa pekee hautasaidia taifa kama vyama hivyo havitakuwa na nguvu ya kufanya kazi ama kuonyesha uzalendo wa kuendesha taifa”. Alisisitiza Mhe. Ahmed.
Kiongozi huyo wa vyama vya sias pia ametoa angalizo kwa jamii kuwa chama cha siasa kinapoanzishwa kiwe ni kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwa kuweka mstakabali mzuri wa vizazi vilivyopo na zijavyo.
Mhe.Ahmed ametoa wito kwa viongozi hao kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa za kuvijengea uwezo vyama hivyo, na kuongeza kuwa mafunzo ya aina hiyo yatasaidia kubadili mawazo na mitazamo ya kiutendaji wa shughuli za vyama vya siasa nchini ili kujielekeza katika mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa.
Baadhi ya mada zilizotolewa nia pamoja na jinsi ya kuendesha chama kama taasisi,utaratibu wa kukagua hesabu za fedha a vyama vya siasa na mambo muhimu ambayo vyama vinapaswa kuzingatia,jinsi ya kuandaa taarifa za fedha kwa ajili ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
Viongozi wa kitaifa wa vyama pia walipata fursa za kufahamu jinsi ya kuandaa rejista ya mali za chama na kuandika taaarifa za mali, jinsi ya kuandaa bajeti ya chama cha siasa na taarifa ya utekelezajii wake na pia wajibu na majukumu ya kufanya marejesho ya wadhamini RITA
Mafunzo hayo yalikuwa mwendelezo wa Mafunzo ambayo Ofisi ya Msajili inaendelea kuyatoa kwa vyama vya siasa ili kusaidia vyama hivyo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kujiendesha kama taasisi.