WAJUMBE WA BODI ZA WADHAMINI ZA VYAMA VYA SIASA WAFUNDWA
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekutana na wajumbe wa Bodi za Wadhamini za Vyama vya Siasa katika kikao kilichofanyika leo siku ya Jumanne ya tarehe 29 Mei, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es salaam, kilichokuwa na lengo la kuwajengea uwezo wajumbe hao katika kutekeleza ipasavyo Sheria ya Vyama vya Siasa katika mapato na matumizi ya vyama vyao .
Akifungua kikao hicho, Bw.Sisty Nyahoza ambaye ni Msajili Msaidizi akimwakilisha Msajili wa Vyama vya Siasa Mhe. Jaji Francis Mutungi, amewaalika wajumbe kushiriki kikamilifu katika kikao hicho ili kuleta tija iliyokusudiwa.
Wakati wa kikao hicho, mada mbalimbali zimewasilishwa zikiwemo mada kuhusu wajibu wa Chama cha Siasa kutunza na kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa taarifa za mapato na matumizi ambayo imewasilishwa na Msajili Msaidizi wa Vyamavya Siasa Bw. Sisty Nyahoza .
Mada zingine zilizowasilishwa ni pamoja na mada kuhusu Wajibu wa Bodi za Wadhamini wa Vyama vya Siasa katika masuala ya fedha ambayo imewasilishwa na Bw. Eliuzeus Kalugendo ambaye ni mwakilishi kutoka Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali (ACGEN).
Na mada kuhusu wajibu na majukumu ya wadhamini iliwasilishwa Bw. Joseph Mwakatobe, mwakilishi kutoka Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Wajumbe pia wamepata fursa ya kuelimishwa kuhusu majukumu ya Bodi za Wadhamini wa Vyama vya Siasa katika ukaguzi wa hesabu za chama, mada iliyowasilishwa na Bw.Benja Majura, mwakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAO).
Kikao hicho ni moja kati ya jitihada za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha vyama vya siasa vinatekeleza ipasavyo Sheria ya Vyama vya Siasa na hasa kuhusu masuala ya mapato na matumizi ya vyama vya siasa, ili kuimarisha demokrasia ya vyama vingi nchini.