Msajili Aipongeza CHADEMA kwa Kuonesha Ukomavu wa Demokrasia Nchini

Habari na: ORPP
Msajili wa Vyama vya Siasa amekipongeza Chama cha CHADEMA kwa kudumisha Demokrasia nchini. Pongezi hizo ziliwasilishwa na Msajili Msaidizi Usajili na Ufuatiliaji wa Vyama vya Siasa, Ndg. Sisty Nyahoza alipokuwa akimwakilisha Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. Jaji Francis Mutungi katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika tarehe 21 Januari 2025 katika Ukumbi wa Mikutano Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Nyahoza alisema, jukumu la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni kuhudhuria mikutano mikuu ili kuhakikisha chaguzi na teuzi zinazofanywa zinafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa Sura 278 na Kanuni za Vyama vya Siasa, lengo kuu ikiwa ni kuhakikisha demokrasia nchini inadumishwa na vyama vya siasa vinazingatia Sheria za nchi na Kanuni zake kwa kuwa vyama vya siasa ni Taasisi za umma. Aliendelea kusema, Mhe. Mwenyekiti, Aikaeli Mbowe nikupongeze umeonyesha ukomavu wa wazi wa kidemokrasia. Alimalizia kwa kusema, kwa namna ambavyo mambo yanavyoendelea, ni wazi kuwa chama hicho kimeelewa dhana ya 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Mhe. Juma Khatibu akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya vyama vyote vya siasa nchini ambavyo vilialikwa, alisema Mkutano huu ni muhimu kwa CHADEMA na alitoa rai kuwa utafanyika kwa amani ili kuendelea kudumisha umoja na mshikamo miongoni mwa wanasiasa nchini. Na vyama vya siasa vimesema viko pamoja na CHADEMA katika kipindi hiki cha uchaguzi, hivyo niwatakieni kheri mmalize salama mkutano wenu na kudumisha umoja, alimaliza.
CHADEMA inafanya Mkutano Mkuu ikiwa ni kutimiza takwa la Sheria ya Vyama vya Siasa, na Katiba yake, sambamba na Kanuni walizojiwekea ambapo pamoja na Mkutano huo ambao ni wa Uchaguzi wa Viongozi wa Kitaifa kwa ngazi za Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar na Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho ulitanguliwa na chaguzi za Mabaraza ya chama hicho ngazi ya Taifa pia.