JAJI MUTUNGI ATOA SALAMU ZA POLE KWA FAMILIA YA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA BARAZA LA VYAMA VYA SIASA
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mhe. Jaji Francis S. K Mutungi leo amefika nyumbani kwa kaka wa Marehemu Peter Kuga Mziray aliyefariki jana katika hospitali ya Rabininsia Tegeta Jijini Dar es Salaam, na kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki waliofika katika msiba huo.
Akizungumza na kaka wa marehemu Bw. John Mziray, Jaji Mutungi amesema kuwa Marehemu Peter Kuga Mziray ni miongoni wa wanasiasa ambao wametoa mchango katika siasa ya vyama vingi nchini.
Wakati wa uhai wake, Marehemu Peter Kuga Mziray aliwahi kuwa Mwenyekiti wa pili wa Baraza la Vyama vya Siasa kwa vipindi viwili kuanzia mwaka 2012 hadi Novemba, 2016.Aliwahi pia kuwa mwanachama na kiongozi wa ngazi ya kitaifa katika Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) na baadaye yeye na wenzake, waliamua kuanzisha chama chao kilichoitwa African Progressive Party of Tanzania (APPT- Maendeleo) tarehe 04 Machi, 2003 ambacho alikuwa Rais Mtendaji wa chama hicho kuanzia kuazishwa kwake hadi kilipofutwa rasmimwaka 2016.
Katika mwaka 2005, Mziray aligombea urais kupitia chama cha APPT – Maendeleo na alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, na Kiongozi wa Vyama visivyokuwa na wabunge ndani ya Bunge hilo. Peter Kuga Mziray alizaliwa tarehe 10 Oktoba 1959 wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro.