Juu yetu

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilianzishwa mwaka 1992 baada ya kutungwa Sheria Namba 5 ya mwaka 1992, na kuanza kutumika tarehe 1 Julai 1992. Kabla ya kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa mwaka 1992, vyama vya siasa wakati wa mfumo wa vyama vingi na hata wakati wa mfumo wa chama kimoja vilikuwa vinasajiliwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kijamii Wizara ya Mambo ya Ndani kwa upande wa Tanzania Bara na Sheria ya Usajili wa Mirathi na Ardhi kwa Tanzania Zanzibar.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni idara ya Serikali inayojitegemea ambayo kiutawala ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ofisi hii ni Taasisi huru katika utendaji na maamuzi yanayohusu majukumu yake kisheria. Hata hivyo, katika kutekeleza majukumu yake, Msajili anatakiwa kushauriana na Waziri mwenye dhamana na masuala ya vyama vya siasa, ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kutokana na muundo wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliopo sasa, majukumu haya hutekelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge kwa niaba ya Waziri Mkuu. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria ni wa mwisho na hauwezi kukatiwa rufaa mahakamani. Hata hivyo, mtu yeyote hakatazwi kuiomba mahakama kupitia na kujiridhisha kama uamuzi husika wa Msajili ulifanywa kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo.

Usajili wa vyama vya siasa ni mojawapo ya masuala ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya 4(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Hivyo, Sheria na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni mojawapo ya masuala ya Muungano, kwa maana ya kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inafanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar.

 
 
Follow Us: